Mbunge Tim Wanyonyi Akemea Utekaji Nyara na Athibitisha Nafasi ya ODM Kama Upinzani

Nairobi, Kenya
Mbunge wa Westlands, Hon. Tim Wanyonyi, alizungumza kwenye KBC Radio Taifa asubuhi ya leo kuhusu masuala muhimu yanayoathiri nchi, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara wa raia, nafasi ya ODM serikalini, na azma yake ya kugombea ugavana wa Nairobi mwaka wa 2027.

Utekaji Nyara wa Raia
Wanyonyi alikashifu vikali vitendo vya utekaji nyara ambavyo vimekithiri nchini, akisema:
“Kama watu wanaotekwa ni polisi, kwa nini wanavaa hoods na nguo za kiraia? Polisi wanapaswa kuwajibika au kutuambia ni nani hawa wahalifu kama si sehemu ya serikali.”

Mbunge huyo alimtetea Waziri wa Baraza la Mawaziri, Justin Muturi, ambaye hivi majuzi alilalamikia kutekwa kwa mwanawe:
“Muturi alikuwa na haki ya kuonyesha kutoridhika kwake. Hili si jambo la kunyamazia. Utekaji nyara wa aina hii ni mbaya zaidi kuliko hata wakati wa utawala wa Rais Moi ambapo watu walitiwa kizuizini na ilijulikana walikopelekwa.”

Aliongeza kuwa vitendo hivi vinatoa sura mbaya kwa serikali na vinakiuka haki za kibinadamu kama ilivyoainishwa kwenye katiba.

Nafasi ya ODM Serikalini
Wanyonyi alisisitiza kuwa ODM haiko serikalini, akisema:
“Maoni ya baadhi ya wanachama wa ODM kuwa tuko serikalini ni ya kibinafsi. Tuliteuliwa ili kufanya serikali kuwa ya uwakilishi mpana, lakini ODM lazima ibaki na utambulisho wake wa kupigania haki za wananchi.”

Alisema chama hicho kitaendelea kuunga mkono sera nzuri lakini kupinga sera zinazowaumiza Wakenya. Aidha, alikanusha uwepo wa makubaliano yoyote kati ya ODM na UDA kuelekea uchaguzi wa 2027.

Azma ya Ugavana wa Nairobi
Wanyonyi alitangaza azma yake ya kugombea ugavana wa Nairobi katika uchaguzi wa 2027, akisema:
“Nilikuwa kwenye kinyang’anyiro cha City Hall mwaka wa 2022 na ningeshinda kama si mipango ya Azimio. Nitaendelea kufuatilia ajenda zangu za kuboresha jiji la Nairobi, na wakati mwafaka ukifika, nitarejea.”

Alikosoa vikali uongozi wa City Hall, akisema kuwa ukusanyaji wa ushuru umepewa kipaumbele kuliko utoaji wa huduma:
“Hakuna kinachofanya kazi Nairobi. Masoko ni machafu, na wafanyabiashara wananyanyaswa bila kupewa mbadala.”

Umuhimu wa Sauti za Vijana na Wakenya
Wanyonyi alitetea kauli ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwamba vijana wanapaswa kusimama na kutetea haki zao, akisema:
“Vijana wana haki ya kudai fursa na huduma bora kutoka kwa serikali. Hakukuwa na uchochezi wowote katika matamshi ya Uhuru. Serikali inapaswa kusikiliza wananchi badala ya kuwa na kiburi.”

Mbunge huyo pia alionya dhidi ya kukandamiza uhuru wa kujieleza, akisema kuwa serikali inapaswa kukubali maoni tofauti yanayotolewa na wananchi.

ODM imeendelea kufanya uchaguzi wa ngazi za mashinani, na Wanyonyi alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kuwa imara kwa ajili ya uchaguzi wa 2027.

Share

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *